Tahariri
##plugins.themes.academic_pro.article.main##
Abstract
Historia imeonyesha kuwa Kiswahili ni mojawapo ya lugha za ulimwengu yenye dhima na nafasi muhimu katika jamii. Si ajabu shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) katika kikao chake cha 41 lilitangaza siku kuu ya Kiswahili duniani kuwa Julai tarehe 7 na kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika kutunukiwa nafasi kama hii. Hii ni kutokana na dhima ambayo imekuwa ikitekelezwa kama lugha ya mawasiliano katika miktadha rasmi na isiyo rasmi. Majukumu haya yametekelezwa katika jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo ndiyo kitovu cha lugha hii, barani Afrika na ulimwenguni kote. Kufikia sasa Kiswahili hakisemwi tu bali pia hufundishwa kama somo katika vyuo vikuu katika mataifa mbalimbali yakiwemo Marekani, Uingereza na Ujerumani. Hali hii ni ithibati tosha ya makini inayohitajika katika ukuzaji wa lugha ya Kiswahili ili kudumisha viwango vya lugha ya ulimwengu. Njia mwafaka ni kutekeleza utafiti katika Kiswahili na kusambaza matokeo ya tafiti hizo kwa njia za makongamano, warsha na machapisho ambayo yatahamasisha na kuitangaza zaidi lugha ya Kiswahili. Kwa upande mwingine waunda mitaala wanastahili kukipa Kiswahili hadhi na nafasi inayostahiki katika mfumo wa elimu. Kiswahili ni lugha ya Kiafrika iliyo katika mstari wa mbele na hatuna budi kukifundisha kama somo la lazima katika viwango vyote vya elimu ili kuwezesha ukuzaji na maenezi yake kwa njia mwafaka.
Jarida la Kiswahili sanifu linatoa fursa nzuri kwa wasomi na washikadau mbalimbali kukuza midahalo, kueneza taarifa na matokeo ya tafiti mbalimbali kuhusu lugha ya Kiswahili ili kuiweka katika nafasi yake stahiki ulimwenguni. Tunatoa shukrani za dhati kwa wahariri, wasomaji na waandishi kwa michango yenu ya thamami kwa jarida hili.
##plugins.themes.academic_pro.article.details##
This work is licensed under a Creative Commons Attribution-NonCommercial-ShareAlike 4.0 International License.