Maadhimisho ya Siku kuu ya Kiswahili Duniani: Upi mwelekeo mwafaka?

##plugins.themes.academic_pro.article.main##

Frida Miruka
Ernest Mohochi
Pamela Ngugi
Juliet Jagero

Abstract

Lugha ya Kiswahili ni mojawapo ya lugha za Kiafrika zinazozungumzwa zaidi ulimwenguni ikiwa na zaidi ya wasemaji Millioni 250.  Hali hii pamoja na hadhi na dhima ya Kiswahili katika jamii mbalimbali ilipelekea shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) katika kikao chake cha 41 kutangaza Julai tarehe 7 kuwa siku kuu ya Kiswahili duniani. Hatua hii ilikifanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika kutambuliwa na Umoja wa Mataifa na kuwa na siku maalum ya kuadhimishwa.  Katika maadhimisho ya tatu yaliyofanyika mwaka 2024 kote duniani, Jumuia ya Afrika mashariki kupitia Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA) iliandaa sherehe nchini Kenya kwa kushirikiana na Wizara ya Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Turathi. Wadau waliohusishwa walikuwa baadhi ya wanataaluma, wapenzi wa lugha ya Kiswahili na Jamii ya Waswahili mjini Mombasa. Maadhimisho haya hata hivyo hayakuwahusisha wadau wote ambao wamechangia kuiinua lugha hii na kuipa sura ya Lugha ya Ulimwengu. Baadhi yao ni wataalamu kutoka vyuo vikuu mbalimbali, waandishi wa vitabu, wanahabari na walimu wa Kiswahili. Mipango ya kuandaa sherehe katika baadhi ya vyuo maalumu haikufua dafu huku vyuo vingine vikiadhimisha siku hii kando na sherehe iliyoandaliwa na KAKAMA. Kukifungia Kiswahili katika jamii na utamaduni wa Waswahili pia kunaishusha hadhi lugha hii kama lugha ya Ulimwengu. Swali linalozuka ni Je, pana haja ya kuweka mpango mwafaka wa kuadhimisha siku hii?  Makala hii inaangazia nafasi ya Kiswahili katika jamii na kutathmini Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili kwa lengo la kupendekeza mikakati ya kuyaimarisha ili kujenga taswira ya lugha ya Kiswahili kama lugha ya ulimwengu. Pendekezo kuu la Makala hii ni kuhimiza ushirikiano wa wadau wote katika maadhimisho ya Siku kuu ya Kiswahili duniani.


 

##plugins.themes.academic_pro.article.details##