Changamoto na suluhu za usimilishaji wa vielelezo katika fasihi ya watoto: mfano kutoka wasifu wa Mwana Kupona wa King’ei (2008)
##plugins.themes.academic_pro.article.main##
Abstract
Makala hii imechunguza changamoto na suluhu zinazotokana na vielelezo vilivyosimilishwa katika Wasifu wa Mwana Kupona (King’ei, 2008). Tafiti kuhusiana na usimilisho wa vielelezo zimefanywa katika hadithi za watoto za Kiswahili. Kwa mfano, Mwendwa (2020) na Mwendwa na wenzake (2021) walichanganua usimilisho wa vielelezo na aina za vielelezo viliyotumika katika hadithi za watoto. Ni dhahiri kwamba, nyingi ya tafiti hizi za awali hazijahusisha moja kwa moja hadithi ya Wasifu wa Mwana Kupona (2008) na changamoto zinazoibuka katika harakati ya kusilimilisha vielelezo. Ni muhimu kuonyesha kuwa katika harakati ya usimilishwaji, changamoto fulani hutokea. Ni katika msingi huu ndipo makala hii imeshughulikia changamoto na suluhu za usimilishwaji wa vielelezo katika Wasifu wa Mwana Kupona. Makala hii imeongozwa na Nadharia ya Usimilisho ya Bluestone (1957) iliyoendelezwa na Goodman (1976), Andrew (1984) na Starrs (2006). Nadharia ya Usimilisho inahusu uzalishaji wa kazi nyingine huru baada ya kazi ya awali kuzalisha kazi nyingine. Data iliyotumika katika makala hii imetolewa maktabani. Mathalan, majarida, tasnifu, na vitabu vinavyohusiana na makala hii yalisomwa. Vilevile, usomaji, uchambuzi na hata unakili wa vipengele muhimu vinavyohusiana na hadithi teule ulifanywa. Matokeo ya utafiti yalibainisha kuwa, changamoto za vielelezo vilivyosimilishwa vinaweza kutokana na mchoraji wa vielelezo vya fasihi ya watoto, uwiano wa picha na matini, usawiri wa wahusika kupitia vielelezo, mandhari katika hadithi na matumizi ya rangi. Aidha, imebainika kuwa vielelezo vinaweza kutumika kupasha ujumbe iwapo vitatumika kwa njia faafu.
##plugins.themes.academic_pro.article.details##
This work is licensed under a Creative Commons Attribution-NonCommercial-ShareAlike 4.0 International License.